Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefanya mabadiliko katika Sekretarieti ya chama kwa kuwaondoa baadhi ya viongozi na kuteua wengine wapya kushika nafasi mbalimbali za uongozi.Mabadiliko hayo yametangazwa leo Jumatano, Julai 29, 2026, baada ya kikao cha NEC kilichofanyika Zanzibar chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, akichukua nafasi ya John Mongella.
Mwanri, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Siha mkoani Kilimanjaro, anafahamika kwa kauli yake maarufu ya "Mzee wa Soma" aliyoitoa wakati wa ukaguzi wa miradi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, kauli iliyopata umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii.
Kwa upande wa Zanzibar, Abdi Mohamed Abdi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, akichukua nafasi ya Dk. Mohammed Said Mohammed maarufu kama "Dimwa". Kabla ya uteuzi huo, Abdi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar.
Katika mabadiliko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Idara ya Organizesheni, akimrithi Issa Haji Gavu, ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka, Zanzibar.
Uteuzi wa Paul Chacha unamaanisha nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora imebaki wazi na inatarajiwa kujazwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia uteuzi mwingine.
Aidha, aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Idara ya Uchumi na Fedha, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Joshua Mirumbe.