Boda boda FC yaichabanga Polisi Jamii Nyang'hwale 2-0 | Icon Communications

Sunday, August 2, 2026

Boda boda FC yaichabanga Polisi Jamii Nyang'hwale 2-0

  Icon Communications       Sunday, August 2, 2026


Na Paul Kayanda, Nyang'hwale. 

Timu ya soka ya waendesha piki piki wilayani Nyang'hwale (Boda boda FC), imeifunga timu ya Polisi Jamii ya wilayani humo 2-0, katika mchezo wa fainali ya kombe la King Mnyama Super Cup, na kufanikiwa kutwaa kombe hilo.


Mchezo huo ulifanyika katika uwanja wa Sabasaba mjini humo, jana Jumapili, Agosti 2, 2026, na kushuhudiwa na mamia ya mashabiki wa mchezo huo waliofurika kwa wingi na kuujaza uwanja huo. 


Magoli ya washindi yalipatikana dakika ya 14 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa mchezaji Michael Kasalenge aliyefunga kwa shuti kali, huku goli la pili likipatikana dakika ya 62 ya mchezo likiwekwa kimiani na mchezaji mkongwe Mgeta Mgeta aliyefunga kwa kichwa.


Dakika za mwisho za kipindi cha pili, timu ya Polisi Jamii ilipata mkwaju wa penati baada ya mchezaji wake kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari, lakini mpigaji alishindwa kufunga baada ya kupanguliwa na mlinda mlango wa timu ya Boda boda.


Mwandaaji na mdhamini mkuu wa michuano hiyo Joseph Donald, almaarufu King Mnyama ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Mwamakiliga uliomo wilayani humo, alisema lengo la michuano hiyo ni kujenga uhusiano mwema kati ya mgodi huo na jamii inayowazunguka.


"Tulianzisha michuano hii kwa lengo la kujenga na kukuza umoja na ushirikiano mwema kati yetu sisi wachimbaji wa Mgodi wa Mwamakiliga na jamii ya watu hapa Kharumwa ili kuleta maendeleo endelevu", alifichua Donald.


"Lakini pia michuano hii inalenga kuibua vipaji kwa vijana wa wilaya ya Nyang'hwale ili kuwasaidia kupata ajira kupitia mchezo huu wa soka kwani siku hizi soka linaajiri vijana wengi", alibainisha Donald.


Donald alitoa wito Kwa wadau wengine wa michezo wilayani humo kuunga mkono juhudi zake kwa kuongeza udhamini ili kuifanya michuano ivutie timu nyingi zaidi na hivyo kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa ya kuonesha vipaji.


Nae mdhamini mwenza wa michuano hiyo, Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Nyang'hwale ASP Mariam Mudo alisema lengo la Jeshi la Polisi wilayani humo kudhamini michuano hiyo ni kuhamasisha jamii kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu.


" Lengo letu kama jeshi la polisi wilaya ya Nyang'hwale kushiriki na kudhamini michuano hii ni kuhamasisha jamii yetu ya hapa hususani vijana kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii yetu", alifafanua ASP Mudo.


Afande Mudo alitoa wito kwa vijana wengi zaidi kujiunga na kushiriki kwa wingi katika shughuli za michezo ilikusaidia kuzuia uhalifu katika jamii.


Pamoja na kutwaa kombe la michuano hiyo, pia timu ya Boda boda ilipata zawadi ya fedha taslimu shilingi 1 milioni, huku timu ya Polisi Jamii ikijiliwaza kwa zawadi ya kitita cha fedha taslimu shilingi laki tano.


Timu ya Isonda iliyoshika nafasi ya tatu ya michuano hiyo ilijinyakulia fedha taslimu shilingi laki tatu.


Mbali na mchezo wa mpira wa miguu, pia kulikuwa na mchezo wa mpira wa Pete, ambao ulizijutanisha timu za Watumishi Nyang'hwale na Kharumwa Queens, ambapo timu ya Kharumwa Queens ilifanikiwa kushinda na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo na kuzawadiwa fedha taslimu shilingi laki tatu.


Nayo timu ya Watumishi iliyoshika nafasi ya pili ya michuano hiyo ilizawadiwa fedha taslimu shilingi laki mbili.






logoblog
Previous
« Prev Post