MADAKTARI BINGWA KUPIGA KAMBI GAKALA, HUDUMA ZA KIBINGWA KUSOGEZWA MBOGWE | Icon Communications

Wednesday, August 12, 2026

MADAKTARI BINGWA KUPIGA KAMBI GAKALA, HUDUMA ZA KIBINGWA KUSOGEZWA MBOGWE

  Icon Communications       Wednesday, August 12, 2026



 Na Paul   Kayanda, Mbogwe


HOSPITALI ya Gakala iliyopo kijiji cha Masumbwe, Kata ya Bukandwe wilayani Mbogwe, mkoani Geita, inatarajia kuwa mwenyeji wa kambi maalumu ya madaktari bingwa itakayotoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi kuanzia Agosti 17 hadi 21, 2026.


Kambi hiyo inalenga kuwawezesha wananchi wa Mbogwe pamoja na maeneo ya jirani kupata huduma za kibingwa karibu na makazi yao, badala ya kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufuata huduma hizo katika hospitali nyingine huko Kasosobe ama katikà Manispaa ya Kahama. 


Akizungumza na jopo la waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Gakala, Bunga Dadu Gakala, alisema hospitali hiyo imeandaa kambi hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika huduma za afya za kibingwa.


Gakala alisema jumla ya madaktari bingwa watakaoshiriki katika kambi hiyo watahudumia wagonjwa wa maeneo mbalimbali, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata uchunguzi na matibabu.


“Hospitali ya Gakala inawatangazia wakazi wa Masumbwe kuwa kutakuwa na madaktari bingwa kuanzia Jumatatu tarehe 17 mpaka 21 mwezi huu.


Tutapokea madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, watoto, upasuaji, mifupa na magonjwa ya ndani kama vile kisukari, presha pamoja na magonjwa mengine ya ndani,” alisema Gakala.


Alisema hospitali hiyo inawakaribisha wananchi wa Masumbwe, wilaya ya Mbogwe na maeneo ya jirani kufika hospitalini hapo ili kutumia fursa hiyo kupata huduma za madaktari bingwa.


Kwa upande wa huduma kwa kina mama, Gakala alisema madaktari watatoa huduma zinazohusu afya ya uzazi, ushauri na vipimo kabla ya ujauzito, matatizo ya kutopata mtoto, uangalizi wa afya wakati wa ujauzito pamoja na huduma za ultrasound kwa wajawazito na wasio wajawazito.


Huduma nyingine zitakazotolewa ni uchunguzi wa matatizo ya kutokwa na uchafu au damu isiyo ya kawaida sehemu za siri, matibabu ya uvimbe katika nyonga au tumbo, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na matatizo yanayohusiana na hedhi na ukomo wa hedhi.


“Pia madaktari hao watatoa matibabu ya uvimbe katika nyonga au tumbo, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matatizo yatokanayo na hedhi na ukomo wa hedhi,” alifafanua.


Mkurugenzi huyo alisema kambi za madaktari bingwa zimekuwa sehemu ya utaratibu wa Hospitali ya Gakala, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya kwa urahisi na karibu na maeneo yao.


Alisema utaratibu huo pia unasaidia kupunguza mzigo wa wananchi kusafiri kwenda mbali kutafuta huduma za kibingwa, jambo ambalo huongeza gharama za usafiri na mahitaji mengine kwa wagonjwa na ndugu zao.


Gakala amewataka wananchi wenye mahitaji ya huduma hizo kutumia kikamilifu siku hizo tano za kambi na kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata uchunguzi, ushauri na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa.









logoblog
Previous
« Prev Post