PSSSF NA TBN WAJENGA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KUPANUA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII | Icon Communications
  • About
  • Facebook
  • Contact
  • Disclaimer

Icon Communications

  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Michezo
  • Burudani
  • Matukio
  • Magazeti

Monday, September 7, 2026

Home » Habari. » PSSSF NA TBN WAJENGA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KUPANUA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII

PSSSF NA TBN WAJENGA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KUPANUA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII

  Icon Communications       Monday, September 7, 2026



Dar es Salaam


Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) wamekubaliana kujenga ushirikiano wa kimkakati unaolenga kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.



Hatua hiyo imefuatia ziara rasmi ya timu ya maofisa wa PSSSF katika Makao Makuu ya TBN yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ambako ilifanya mazungumzo na viongozi wa mtandao huo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa habari, uelimishaji wa umma na usambazaji wa taarifa sahihi kupitia majukwaa ya kidijitali.


Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye wanachama zaidi ya 200 nchi nzima na Diaspora, upo tayari kutumia uwezo, uzoefu na wigo wa majukwaa ya wanachama wake kutoa elimu sahihi kuhusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na PSSSF.


Hata hivyo, Msimbe alisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupatiwa mafunzo ya kina kuhusu shughuli, huduma na uendeshaji wa mfuko huo, ili waweze kuielimisha jamii kwa usahihi na ufanisi zaidi.


Alisema ushirikiano huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo waliopo katika maeneo ambayo taarifa kuhusu hifadhi ya jamii na mifumo ya pensheni hazijawafikia kwa kiwango cha kutosha.


Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii.


Njaidi aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi, mapendekezo na hoja zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi. Alisema dhamira ya PSSSF ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii pamoja na uwekezaji unaofanywa na mfuko kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.


Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, amesema mtandao huo una historia kubwa katika maendeleo ya habari za kidijitali nchini na unajivunia kuwa na wanachama wenye weledi, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali.


Michuzi amesema TBN ilianzishwa kwa dhamira ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vizuri katika medani za kidijitali, kwa kusambaza taarifa sahihi zinazochochea maendeleo na kusaidia kutanua gurudumu la uchumi wa Taifa.


“TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Michuzi.


Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo upo tayari kutumia waandishi wake mahiri na majukwaa mbalimbali ya wanachama wake kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zenye kuaminika na zitakazowawezesha kuelewa vyema haki, wajibu na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.


Ameongeza kuwa ushirikiano wa PSSSF na TBN unaweza kuwa daraja muhimu la kuunganisha taasisi hiyo na wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho majukwaa ya kidijitali yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya habari na maarifa.


Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.


Kwa upande wa TBN, mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi













logoblog
Previous
« Prev Post
Next
Next Post »
Imechapishwa na Icon Communications Published at September 07, 2026

Tafuta Habari

ZILIZOSOMWA SANA

  • Breaking : HAYA HAPA MATOKEO YA MTIHANI DARASA LA SABA 2026
    TAZAMA MATOKEO HAPA
  • BREAKING!!! HAYA HAPA MATOKEO YA MTIHANI KIDATO CHA NNE 2025
    BOFYA KUTAZAMA MATOKEO BOFYA KUTAZAMA MATOKEO
  • Hii hapa bei ya petroli, dizeli na Mafuta ya taa Disemba 2025 Nchini
       
  • JESHI LA UHAMIAJI NCHINI LATANGAZA NAFASI ZA KAZI
     
  • MAGAZETI YA LEO JUMATANO JULAI 15,2026
  • RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI USIKU HUU, UMMY AKUMBUKWA
     
  • TAMISEMI YATANGAZA SELECTION ZA KIDATO CHA TANO, VYUO VYA KATI 2026/2027
      Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Imetangaza machaguo "selection" za wanafunzi wa kidato cha ...
  • MAGAZETI YA LEO ALHAMISI FEBRUARI 19, 2026
                                       
  • EWURA YATANGAZA BEI ZA MAFUTA FEBRUARI 2026, DIZELI YASHUKA MARADUFU
    Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa  za mafuta aina ya petroli zitakazotumika hapa nch...
  • EWURA YATANGAZA BEI MPYA YA MAFUTA KWA MWEZI SEPTEMBA 2026
Copyright © Icon Communications. All rights reserved.